KABURU: KIPIGO CHA YANGA KINAUMA
MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kitendo cha timu yao kufungwa na Yanga juzi kimewaumiza, lakini hakiwarudishi nyuma, wanachukulia ni sehemu ya mchezo.
Simba ilipata kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo uliochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kipigo ambacho kimesababisha klabu hiyo kumlaumu mwamuzi aliyekuwa akichezesha Israel Nkongo kwa madai kuwa hakutenda haki.
Licha ya Nyange kudai kuwa wanasonga mbele kujipanga na michezo ijayo kwa ajili ya kufanya vizuri, tayari msemaji wao, Haji Manara alitangaza jana kupeleka barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumlalamikia mwamuzi huyo kwa kushindwa kutenda haki.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Nyange alisema kipigo hicho kinauma sana, lakini anaamini kikosi chao ni kizuri na kilijituma uwanjani kwa uwezo wake, kwani yaliyotokea uwanjani wanayaacha kama yalivyo.
“Ni kweli tulifungwa na hatukufurahia hilo kwa sababu tulidhamiria kufanya vizuri, lakini hatujakata tamaa kwani huo ni mchezo mmoja, tunaangalia mbele kwa michezo ijayo,” alisema Kaburu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa TFF.
Alisema baada ya mchezo huo anaamini Kocha Mkuu Dylan Kerry atafanyia kazi mapungufu katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kufanya vizuri katika michezo ijayo. Nyange alisema zipo mechi nyingi mbele wanahitaji kushinda na kutimiza kile walichokusudia katika kulichukua taji la ubingwa wa ligi na kushiriki michuano ya kimataifa.
Kipigo hicho kimeishusha Simba kutoka nafasi ya pili hadi ya nne kwenye msimamo wa ligi. Simba wanatarajiwa kucheza dhidi ya Stand United ya Shinyanga katika mchezo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments