Header Ads

MALINZI AZINDUA ROCK CITY MARATHON

MWENYEKITI wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi amezindua msimu wa saba wa mbio za Rock City Marathon zitakazofanyika Novemba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mbio za Rock City Marathon zinazoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI), kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania (RT), pamoja na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MRAA), zinalenga kutambua na kuinua vipaji vya wanariadha nchini na pia kukuza utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jana Dar es Salaam, Malinzi alisema baraza lake lina furaha kuona kampuni binafsi zikijiingiza katika kuinua mchezo wa riadha nchini.
“Mchezo wa riadha una changamoto kubwa na tunatambua jitihada zinazoendelea kufanywa na kampuni ya Capital Plus katika kurudisha hadhi ya mchezo huu nchini kama ilivyokuwa miaka ya sabini na themanini,” alisema Malinzi ambaye ni mfanyabiashara maarufu nchini.
Alisema Tanzania itarudi kileleni katika medani za michezo duniani kama wachezaji wataandaliwa katika viwango vinavyokubalika kimataifa. “Inashangaza kuona taifa la watu milioni 45 linawakilishwa na wanariadha wachache sana, tena katika mbio ndefu huku tukikosa wanariadha wanaoliwakilisha vyema taifa katika mbio fupi,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu kutoka Kampuni ya Capital Plus International, Erasto Kilawe alisema mbio hizo zimekuwa zikionesha mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009. “Jiji la Mwanza limebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii.
Jambo hili limetusukuma kuendelea kumulika vivutio vya kipekee vinavyopatikana katika ukanda wa ziwa Victoria kupitia mbio hizi,” alisema Kilawe huku akiongeza kuwa mikakati kabambe imewekwa ili kuhakikisha mbio za mwaka huu zinakuwa za mafanikio makubwa kuliko misimu iliyopita.


Alisema baadhi ya kampuni zimeanza kujitokeza kudhamini mbio hizo ikiwamo Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Precision Air, New Africa Hotel na Bank M huku kampuni zaidi zikionesha nia ya kudhamini mbio hizo.

No comments

Powered by Blogger.