Header Ads

SIMBA YALIA NA MUAMUZI

UONGOZI wa timu ya Simba umemlalamikia mwamuzi Israel Nkongo aliyechezesha mechi yake ya Ligi Kuu bara dhidi ya Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita ukidai hakutenda haki. Mbali na madai hayo, Simba pia imemlalamikia mchezaji wa Yanga Donald Ngoma kwa kumpiga kichwa mchezaji wao Hassan Kessy.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Simba ilichapwa mabao 2-0. Hata hivyo Simba imeipongeza Yanga kwa ushindi huo ikisema imekubali matokeo.



Taarifa ya Ofisa Habari wa Simba Haji Manara kwa vyombo vya habari jana, ilisema: “Tutumie nafasi hii kiungwana kabisa kuwapongeza watani wetu wa jadi kwa ushindi huo walioupata,” alisema.
“Pili tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza mchezo huo salama, na hapa Mungu ashukuriwe sana pamoja na wapenzi wetu pia… sababu mashabiki wetu wameonesha utulivu wa kiunamichezo kwa kutokufanya fujo yoyote licha ya mwamuzi wa mchezo huo Israel Nkongo kuharibu mchezo kwa makusudi,” alisema Manara kwenye taarifa yake.
“Nkongo kwa dhamira ya kusudi jana aliamua kuwatoa wachezaji wetu mchezoni kwa kuanza kugawa kadi kwa wachezaji wetu pasi na sababu na kwa rafu zilezile kuacha wachezaji wa Yanga kucheza bila kuwaonya”.
Manara alisema kilichoshangaza mashabiki wote waliokuwa uwanjani na walioangalia mechi hiyo kwenye runinga ni kumuacha Ngoma kuendelea na mchezo ilhali alimpiga kichwa cha makusudi mchezaji wao Hassan Kessy.
“Mbali ya vitendo hivyo wachezaji wetu wametulalamikia kutukanwa na mwamuzi wa mchezo huo Nkongo”. “Tunaamini TFF watachunguza malalamiko yetu na kuchukua hatua stahiki kwa mwamuzi huyo ambaye kila mtu aliyeuona mchezo huo anakiri kuwa alishindwa kuumudu”.


Alisema kutokana na tukio hilo, Simba imewataka mashabiki wake kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho uongozi wao umeiandikia barua TFF na bodi ya ligi wakiamini haki itatendeka.

No comments

Powered by Blogger.