NANI, ATASHUKA KILELENI?
NANI kushuka kwenye msimamo wa ligi leo? Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar zina kibarua kizito cha kutafuta pointi tatu ambazo zitawafanya kuendelea kung’ara na kujiweka sehemu salama za kugombea nafasi za juu.
Timu 14 kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu wa 2015-16 zitacheza kwenye viwanja tofauti huku kila moja ikiwa na shauku ya kutaka kushinda. Mabingwa watetezi, Yanga ndio wanaoshikilia usukani kwa pointi 12 wakilingana na Azam FC na Mtibwa Sugar, lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa huku Simba ikishika nafasi ya nne.
Yanga wanakutana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Je, watafanikiwa kuvunja mwiko wa kutowafunga Mtibwa uwanjani hapo? Mara ya mwisho walipokutana uwanjani hapo msimu uliopita Yanga walifungwa mabao 2-0. Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm alisema ana matumaini ya kushinda kwani malengo waliyojiwekea ni kushinda kila mchezo. “Tuna imani ya kufanya vizuri katika mchezo wetu na Mtibwa.
Tunataka kuvunja huo mwiko kwani kikosi changu kiko vizuri kwa mapambano,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi. Yanga inahitaji kushinda mchezo huo kama inataka kuendelea kuongoza ligi, na ikiwa itafungwa na Azam FC wakashinda, basi Yanga watashuka hadi nafasi ya tatu au ya nne na kuwaruhusu Mtibwa na Azam kuwa juu yao.
Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema timu yao imejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo. “Tunaichukulia Yanga ni timu ya kawaida haiwezi kututisha. Waje watakiona cha moto,” alisema Kifaru na kuongeza kuwa safari hii ni zamu yao kushinda kwa kila mchezo ulioko mbele yao ili kuchukua ubingwa wa ligi.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi wenyeji watashuka dimbani kuvaana na Coastal Union ya Tanga. Azam FC wamedhamiria kuendeleza rekodi yao ya kutokupoteza mchezo wowote. Tayari wameshinda michezo yote ya ugenini na nyumbani iliyokwisha kucheza hadi sasa.
Mara ya mwisho Azam FC kukutana na Coastal Union Machi mwaka huu, Azam waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Leo zinakutana Azam Complex hivyo bado Azam ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi na kuwafunga Coastal kwa mara nyingine ambao wameanza vibaya ligi wakishikilia nafasi ya 15 kwenye msimamo wakiwa na pointi mbili.
Licha ya ubora wa Azam FC, hawatakiwi kuidharau timu hiyo ya Tanga kwa vile inawafahamu na lolote linaweza likatokea kwa sababu nao wanataka matokeo mazuri. Kwa upande mwingine, Simba wanaikaribisha Stand United ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakitoka kujeruhiwa vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 na watani wao wa jadi, Yanga.
Simba inayoshika nafasi ya nne kwa pointi tisa na Stand United inayoshika nafasi ya tano kwa pointi sita, zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja huo msimu uliopita. Itapania kushinda leo ili kuwathibitishia mashabiki wao kuwa iliteleza tu kwa Yanga.
Mchezo mwingine itakuwa ni Majimaji ya Songea dhidi ya Ndanda FC katika mchezo utakaochezwa mkoani Songea, Ruvuma ikiwa ni mara yao ya kwanza. Majimaji ikishika nafasi ya sita ikiwa na pointi sita wakati Ndanda FC inashika nafasi ya 10 kwa pointi nne. Zote zinahitaji ushindi.
Kwa upande wa Kagera Sugar yenye pointi nne inacheza na JKT Ruvu wanaoshikilia mkia. Kagera Sugar wana nafasi ya kufanya vizuri kwa vile wako nyumbani. Africans Sports itacheza na Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani wakati Tanzania Prisons wataikaribisha Mwadui FC kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

No comments