Header Ads

MAJENGO CHUO CHA TIBA CHA KIJESHI YAKABITHIWA

SERIKALI imekabidhiwa majengo mapya ya Chuo cha Sayansi na Tiba cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi. Akizungumza baada ya makabishidhiano hayo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi (pichani) alisema chuo hicho kitasaidia kuongeza utoaji wa wataalamu wa tiba hususani madaktari.
Alisema chuo hicho chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kwa wakati mmoja kimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 7.2 kwa ufadhili wa serikali ya Ujerumani. “Tunaishukuru serikali ya Ujerumani, kwani mbali na chuo pia wametusaidia kukarabati hospitali kadhaa za jeshi, kuweka vifaa na kutoa hospitali zinazotembea (mobile clinic),” alisema.
Alisema chuo hicho pamoja na kutoa mafunzo kwa watanzania, pia kitazalisha wataalamu wa afya watakaotoa huduma katika hospitali za jeshi na raia. Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Kochanke ambaye aliwakilisha Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, alisema serikali yake imesaidia ujenzi wa chuo hicho ili jeshi liweze kuzalisha wataalamu wa afya.
Alisema serikari yake inathamini mchango wa Tanzania katika kulinda amani kwa kutoa majeshi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Darfur na kwingineko. Mkuu wa chuo, Brigedia Jenerali Dk Luhindi Msangi alisema kwa sasa chuo chake ambacho ni kishiriki cha Muhimbili wako mbioni kukisajili Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

No comments

Powered by Blogger.